Alhamisi , 2nd Nov , 2017

Mahakama nchini Pakistan imemfunga mwanamume mmoja miezi sita jela kwa kuoa mke wa pili bila ya idhini kutoka kwa mke wake.

Mahakama hiyo ya mjini Lahore pia imemuamrisha Shahzad Saqib, kulipa faini ya dola 1,900, na kukataa maoni yake kuwa dini ya kiislamu inamruhusu kuoa hadi wake wanne.

Mke wa kwanza wa Sadiq Ayesha Bibi, alikuwa amefanikiwa kujitetea kuwa kuoa bila idhini yake ulikuwa ni ukiukaji wa sheria za familia nchini Pakistan.

Kwa mujibu wa BBC imeandika kwamba Wanaharakati wa masuala ya wanawake wamesema kuwa kesi hiyo ni pigo kwa ndoa za wake wengi na kuongeza kwamba hukumu hiyo itawapa wanawake zaidi walio katika hali kama hizo motisha ya kupeleka kesi mahakamani.

Inadaiwa kwamba nchini Pakistan, wanaume wanaotaka kuoa wanawake zaidi hufanya hivyo baada ya miaka kadhaa na ni lazima wapate idhini kutoka kwa mke wa kwanza.

Baraza la kiislamu nchini Pakistan ambalo hutoa ushauri wa serikali kuhusu masuala ya kiislamu, mara kwa mara limekosoa sheria za familia nchini humo.

Hata hivyo mtuhumiwa huyo Sadiq ana haki ya kukata rufaa kupinga hukumu hiyo ya siku ya Jumatano.