Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu nchini Tanzania (LHRC) kimesema kuwa kumekuwepo na takwimu nyingi zinazoonesha idadi ya watoto waliofanyiwa vitendo vya ukatili bila ya kuwepo na idadi ya wahalifu waliokamatwana na uhalifu huo hali inyozua hofu kwa watoto.
Katika taarifa iliyotolewa na LHRC inasema kuwa ili kuweza kupambanana na vitendo hivyo ni lazima kuongezwe nguvu katika kupambana na wahalifu wanaotenda makosa hayo kwani utafiti uliofanywa na jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia unaonesha kuwa kwa kipindi cha Januari mpaka Machi matukio ya ukatili yaliongezeka kutoka 180 mpaka 1,765.
Taarifa hiyo imeeleza cha kusikitisha zaidi asilimia 90 ya wahusika wakuu wa matukio hayo ya ukatili ni wanafamilia au ndugu wa karibu wa mtoto husika hivyo wengi huamua kumaliza mambo yao kindugu na kumnyima haki mtoto aliyefanyiwa ukatili.
Aidha, kituo hicho kinaitaka serikali kupitia Bunge kufanya marekebisho ya sheria zote kandamizi kwa watoto na kuhakikisha kuwa sheria zilizopo zinatekelezwa na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaowafanyia watoto vitendo vya ukatili.

