Jumatano , 21st Apr , 2021

Wazabuni wa Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi vya maabara nchini wametakiwa kuzingatia maadili ya biashara ya dawa kwa kuweka mbele suala la uzalendo na ubora ili Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) iendelee kuimarisha uhusiano wa manunuzi uliopo baina yao.

Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Idara Kuu Afya, Prof. Abel Makubi wakati akizungumza na wazabuni wa Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi vya maabara nchini.

Hayo yameelezwa Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Idara Kuu Afya, Prof. Abel Makubi wakati akizungumza na wazabuni hao ambao wanauza na wanasambaza bidhaa hizo kwenda MSD.

Prof. Makubi amesema kuwa moja ya vipaumbele vya Serikali ni kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kutosha na zenye viwango zinazopelekwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili wananchi wapate huduma bora za afya wakati wote na popote.

Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa na vitendanishi vya maabara kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini zinaimarika,hivyo mnatakiwa kuweka mbele uzalendo , uaminifu , uhalisia wa bei na mzalishe bidhaa zenye ubora ili kukidhi matakwa ya serikali na kupunguza gharama za matibabu Kwa wananchi na hata kwa mifuko yetu ya Bima", amesisitiza Prof. Makubi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD Meja Jenerali Dkt. Gabriel Saul Mhidze amewashukuru wazabuni kuendelea kuiamini MSD na kuipa huduma pamoja na ushauri ambao wamekuwa wakimpatia ili kuboresha huduma ya upatikanaji wa dawa nchini.