Jumanne , 10th Jan , 2023

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amewashauri wadau wa maendeleo nchini kuwasaidia wakulima katika uzalishaji na sio kuwapa semina kwa mwaka mzima bila uzalishaji

Bashe ametoa kauli hiyo katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari na wadau wa kilimo ambapo amesema wakulima nchini wamebadilishwa kutoka kuwa wazalishaji na sasa wanazunguka kwenye semina mbalimbali jambo ambalo linashusha uzalishaji

"Tumewabadilisha wakulima kutoka kuwa wazalishaji mpaka kuwa Grants Preneurs, yani mkulima kuanzia Januari hadi Desemba yupo kwenye semina, leo Mbeya kesho huku, atazalisha saa ngapi, huyu anataka umchimbie kisima wewe hizo hela za semina mchimbie kisima" amesema Waziri Bashe

Aidha Waziri Bashe amesema serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha kwenye kilimo hivyo ni wakati wa kuzalisha kwa wingi

"Rais Samia ana utashi wa kisiasa kwa ajili ya kilimo na ana utayari wa kuwekeza fedha kwenye kilimo, na mimi nawaambia wenzengu wizarani, tukifeli kuzalisha tutakuwa hatujawatendea haki wananchi wa nchi hii"

  
Aidha Waziri huyo amewataka wadau wa maendeleo nchini kama wanahitaji kuwekeza nchini waendane na matakwa ya wizara yake huku akisema kama watashindwa ni bora wakaondoka na fedha zao

"Unaweza kumkuta development Partner anakwambia tumeisaidia Tanzania kwenye Kilimo Dola milioni 5, ukiwauliza nini wanasema tumeenda kuwafundisha wakilima, kufanya Policy Analysis, nimewaambia no, nina vipaumbele vyangu vitano kama una pesa cheza na hizi tano huwezi nenda nyumbani na pesa yako"