Ijumaa , 12th Jul , 2024

Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ameeihakikishia sekta binafsi ya Tanzania kuwa atakuwa mtetezi wa kwanza ilikuhakikisha ushindani wa sekta ya viwanda na biashara za kada tofauti.

Dkt. Jafo amesema “Mimi Jafo nitakuwa mtetezi wenu wa kwanza kuhakikisha mnafanya vizuri, hatuwezi kujenga uchumi wa Nchi kama ninyi (sekta binafsi) hamfanyi vizuri”.

Kwenye Kikao hicho viongozi wa Vyama vya Biashara na wakurugenzi wa makumpuni wakiwemo, (TCCIA, CTI, ZNCC, TATOA, TWCC, ACT, TAFOPA, TTMOA, ATE, TBA, TAMIDA, TANEXA, CATA, TASOTA, TASAA, TASSIM, TSA, TWCA, TAA, TUCASA, TEGAMAT n.k) walimuelezea, Waziri Dkt. Jafo changamoto zinazowasibu katika biashara zao, zikiwemo; Ukusanyaji wa kodi kwa nguvu, hasa matumizi ya Hati za uwakala wa ulipaji kodi (Agency Notice) na TRA, Utitiri wa taasisi za urekebu ambazo zinatoza ada mbalimbali, Kufungiwa kwa akaunti za wafanyabiashara na mashine za EFD, Kuongezeka kwa bidhaa za magendo nchini, hivyo kutishia viwanda vya ndani, Kutolindwa kwa viwanda vya ndani, kusababisha kushuka kwa uzalishaji, Gharama kubwa za kufanya biashara na uzalishaji kutokana na ada na tozo mbalimbali, ikiwemo ushuru wa huduma (Service Levy) na ada ya stempu za kielektroniki (ETS).

Mbali na viongozi wa vyama vya Biashara na Wakurugenzi wa makampuni Binafsi, Viongozi wengine waliohudhuria Mkutano huo ni pamoja na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt Hashil T. Abdallah, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania Angelina Ngalula, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Raphael Maganga na Viongozi wengine.

Mkutano huo uliandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa udhamini wa Trademark Africa.