Jumapili , 26th Feb , 2023

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha maisha ya Watanzania hususan vijana kwa kuwawekea mazingira wezeshi ya kujiajiri kupitia shughuli za uvuvi na ukuzaji viumbe maji ili kukuza kipato chao na Taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa wakati wa hafla fupi ya kuzindua programu ya mafunzo atamizi ya uvuvi na ukuzaji viumbe maji kwa vijana iliyofanyika Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani.

Akiongea wakati akizindua programu hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia amedhamiria kuwawezesha vijana kujiajiri na ndio maana katika mwaka huu wa fedha wa 2022/23 ameridhia kutengwa fedha ili vijana 500 waweze kupatiwa mafunzo atamizi ili waweze kujiajiri.

"Mwaka huu tumepanga kuwawezesha vijana 500, awamu hii ya kwanza tumeanza na vijana 200 halafu watafuatiwa na vijana wengine 300, hii programu ni endelevu na mwakani tutaendelea kutenga bajeti, lengo ni kutengeneza vijana watakaokuwa jasiri kukabiliana na mazingira yanayowazunguka",amesema Ndaki