Ijumaa , 31st Mei , 2024

Tanzania na Denmark zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika kutekeleza programu ya maboresho ya mifumo ya kodi.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaabani, akiagana na Waziri wa Kodi wa Denmark, Mhe. Jeppe Bruus, baada ya kikao kando ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jijini Nairobi nchini Kenya.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaabani kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kodi wa Denmark, Mhe. Jeppe Bruus, kando ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Jijini Nairobi nchini Kenya.

Alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Denmark zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika kutekeleza program hiyo ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) chini ya Wizara ya Fedha.

“Tumekubalina kuwakutanisha wataalam wa Tanzania na Denmark kupitia Ubalozi wao ili kufanya tathmini na kuangalia maeneo yote muhimu yanayohitaji maboresho katika kutekeleza program hiyo”, alisema Bi. Amina.

Bi. Amina aliongeza kuwa kupitia wataalamu wa nchi hizo mbili (Tanzania na Denmark), Serikali inatarajia maboresho yatakayofanywa katika program hiyo yatayasaidia kuongeza ufanisi katika makusanyo ya mapato nchini.

Aidha katika kikao hicho Denmark imeelezea maendeleo mbalimbali ya baadhi ya masuala ambayo ilikubaliana na Tanzania kupitia ziara zilizofanywa na Viongozi hivi karibuni.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Kodi wa Denmark, Mhe. Jeppe Bruus alisema Wizara ya Kodi nchini Denmark itaendelea kutoa msaada wa kitaalamu kwa Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha inafanya maboresho ya program mbalimbali za kodi na kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu kati ya nchi hizo mbili.

‘’Serikali ya Denmark kupitia Wizara ya Kodi, inatambua umuhimu wa ushirikiano uliopo kati ya nchi hizi mbili, hivyo ni muhimu kuendeleza ushirikiano huo hasa kwa kusaidia katika eneo la utaalamu wa masuala ya kodi’’, alisema Mhe. Bruus.

Aliongeza kuwa Denmark na Tanzania zina historia ndefu katika masuala mbalimabli ya ushirikiano na kwa sasa nchi hiyo mbali na kuendeleza ushirikiano katika masuala ya kodi, pia inaangazia kukuza ushirikiano katika masuala ya kijamii na kiuchumi.

Katika kikao hicho Waziri wa Kodi wa Denmark, Mhe. Jeppe Bruus alitumia fursa hiyo kujitambulisha na kuelezea uwezo wa Wizara anayosimamia na kuitaka Tanzania kufanya kazi kwa ushirikiano katika sekta hiyo.