Jumapili , 27th Nov , 2022

Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegilo amesema,kuna haja ya Serikali kuanza mchakato wa kutumia maji ya ziwa Nyasa ili kumaliza shida ya maji kwa wananchi,badala ya kuendelea kutegemea vyanzo vya maji ambavyo sio vya uhakika.

Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegilo (kulia)akiwa na mbunge wa Nyasa mhandisi Stella Manyanya.

Kivegilo amesema hayo kwa nyakati tofauti,wakati akikagua ujenzi wa miradi mikubwa ya maji katika kata ya Liuli na Lituhi Halmashauri ya wilaya Nyasa mkoani Ruvuma inayojengwa kwa gharama ya Sh.bilioni 11.3

Kivegilo alisema,hakuna sababu ya wilaya ya Nyasa kuwa na tatizo la maji kwa wananchi wake,kwani kuna vyanzo vingi na uhakika ikiwamo ziwa Nyasa lenye uwezo wa kuhudumia wilaya yote ya Nyasa.

“unaposikia watu wana shida ya maji na wanaishi kando ya ziwa nyasa haiingii akilini hata kidogo,wakati umefika sasa kwa serikali kuanza mchakato wa kutumia maji ya ziwa Nyasa badala ya kuendelea kutegemea vyanzo vingine ambavyo havina uhakika sana”alisema Kivegilo.

Miradi hiyo ni mradi wa maji Liuli unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 5 na mradi wa maji wa Mwerampya kata ya Lituhi unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 6.5.