Ijumaa , 23rd Sep , 2022

Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) limeiomba mamlaka ya mapato Tanzania (TPA) kutoa kadi ya kijani kwa wanachama wake ili kuipa mizigo yake kipaumbele cha kutolewa bandarini haraka.

Bw. Plasduce M. Mbossa, Mkurugenzi Mkuu TPA

Mapema leo Septemba 23, 2022 wajumbe wa baraza la biashara la Afrika Mashariki (EABC) wamekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ili kuona namna ya kuongeza kasi ya upakuaji na usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda katika mataifa yasiyo na bandari ikiwemo Malwai, Zambia, Congo, Burundi, Rwanda na Uganda.

“Sisi ndiyo washikadau mhimu katika bandari ya Dar es Salaam, hivyo baada ya kuteuliwa kwa Mkurugenzi mpya wa TPA tumeona ni vema tukutane na kuzungumza nae ili kujadili changamoto tulizonazo na ni kipi tufanye, mfano hapa bandarini kuna ucheleweshwaji wa upakuaji mizigo na kuutoa mzigo bandarini, tunatumia muda mrefu kukamilisha mchakato, hivyo tumemuomba kwamba sisi wanachama wa EABC ambao ndo wateja wakubwa kwa bandari tupewe kadi ya kijani ambayo itatoa kipaumbele kwa mizigo yetu ili ishughulikiwe haraka inapokuwa bandarini na kuchangamsha biashara"- John Bosco Kalisa, Mkurugenzi Mtendaji  EABC.  

Aidha, kuhusu ujenzi wa bandari ya Bagamoyo Mkurugenzi wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa amesema kuwa mamlaka hiyo na serikali wamepanga kuanza ujenzi wa bandari hiyo kwa pesa zake hata kama mfadhili atachelewa kupataikana na kwamba ikikamilika itaongeza ufanisi wa bandari za Tanzania.

“Hata hivyo ili kuhakikisha kwamba tunawahudumia wateja, suala la Bandari ya Bagamoyo ni mhimu, na mamlaka ya bandari na serikali  tutaanza ujenzi wa bandari ile bila kusubiri mfadhili, ikikamilika ile maana yake ni kwamba foleni katika bandari ya Dar es Salaam itapungua na wafanyabiashara hawatakimbia kwenda nchi zingine"- Plasduce Mbossa,  Mkurugenzi Mkuu TPA.