Ijumaa , 22nd Jul , 2022

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ametoa agizo kwa wawekezaji katika Sekta ya Madini kuendeleza maeneo yao yenye madini ya kimkakati badala ya kuyaacha bila kuyaendeleza suala linalopelekea wenye nia ya kuwekeza kukosa fursa hiyo

Amesema wapo wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika Sekta hiyo maeneo mbalimbali nchini lakini wanashindwa sababu baadhi yao wanakaa na maeneo kwa muda mrefu bila kuyaendeleza.

Hayo yamebainishwa Julai 21, 2022 na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko katika kijiji cha Mgambazi wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma alipotembelea Kampuni ya Lubalisi Resources Ltd inayofanya utafiti wa madini ya Nikeli.

Amewasisitiza wawekezaji katika Sekta ya Madini wanapaswa kufuata Sheria na Taratibu zilizowekwa katika uwekezaji huo ili kuepuka kufutiwa leseni zao.

Aidha, amewataka wawekezaji hao kuwasilisha taarifa za kipindi cha miezi mitatu ya utekelezaji kazi ya utafiti wa madini iliyofanyika kwa kipindi husika (quarterly report) ambayo husaidia kujua mwenendo au maendeleo ya mradi ya utafiti wa madini.

Amesema lengo la taarifa hizo ni kuiwezesha Serikali kutambua maendeleo ya mradi kwa kipindi husika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Hanafi Msabaha amewataka wawekezaji kuchangia katika huduma mbalimbali za kijamii ili jamii zinufaike na uwepo wa madini. Amesema ushirikishwaji wa wananchi utasaidia kupunguza malalamiko yanayojitokeza mara kwa mara kuhusu wawekezaji.

Naye, Mratibu wa Mradi na Mawasiliano ya Jamii Ashery Lemelo amemuakikishia Dkt. Biteko kusimamia maelekezo yaliyotolewa na Serikali katika mradi huo.

Katika wilaya ya Uvinza tafiti zinaonesha kuwa na madini ya Nikeli. Madini hayo hutumika katika utengenezaji wa bidhaa za magari ya umeme ikiwemo betri na vifaa mbalimbali vya umeme. Aidha, madini ya mkakati yenye uhitaji mkubwa nchini ni pamoja na madini ya Kinywe.