Jumatano , 14th Sep , 2022

Benki ya CRDB leo imezindua kampeni maalum ya elimu ya bima ya vyombo vya moto iliyopewa jina la ‘Kuwa Shua’ katika hafla ulifanyika katika gereji ya MacAuto iliyopo Sinza Jijini Dar es salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Bima wa Benki ya CRDB, Moureen Majaliwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)

Akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki ya CRDB, Moureen Majaliwa amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha wamiliki wa vyombo vya moto kukatia vyombo vyao bima ili kujikinga dhidi ya majanga.

Majaliwa alisema pamoja na kuwa bima ya vyombo vya moto ni moja ya bima zinazotumika kwa kiasi kikubwa bado wamiliki wengi wa vyombo vya moto nchini hawana elimu ya kutosha kuhusu bima, jambo linalopelekea wengi kupuuzia.

“Katika kipindi cha kampeni maafisa wetu wa Benki watakuwa wakitembelea wateja kuwapa elimu ya bima za vyombo vya moto, lakini pia tutakuwa tukitoa zawadi kwa wateja watakaokata bima kupitia Benki ya CRDB,” alisema Majaliwa.

Akielezea kuhusu zawadi kwa wateja Majaliwa alisema wamiliki wa vyombo vya moto watakaolipia bima kubwa ya ‘comprehensive’ watarudishiwa asilimia 5 ya kiasi cha bima (kabla ya VAT) kama mafuta kupitia vituo vya Oryx nchi nzima.