TUZO za EATV zimeanzishwa mwaka 2016 na kampuni ya East Africa Television na Radio, zitafanyika kwa mara ya kwanza tarehe 10/12/2016 jijini Dar Es Salaam,Tanzania.
Tuzo hizi zinashirikisha wasanii wa muziki na filamu kutoka nchi za Afrika Mashariki na zitakuwa zikifanyika kila mwaka, huku vipengele vya tuzo vikiongezeka kila mwaka kutoka vipengele kumi vinavyoshindaniwa mwaka huu.
Kuanzishwa kwa tuzo hizi kuna lengo la kuthamini wasanii na kuleta ushindani kwenye sekta hii ya sanaa kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Kwenye tuzo za mwaka huu kutakuwepo na jumla ya vipengele kumi. Vipengele sita vitashindaniwa na wasanii wa muziki, Vipengele vitatu vitashindaniwa na wasanii wa filamu na kipengele kimoja kitakua ni tuzo ya heshima.
Vipengele hivyo kwa upande wa muziki ni mwanamuziki bora wa kiume, mwanamuziki bora wa kike, mwanamuziki bora Chipukizi, kundi bora la mwaka, Video bora ya mwaka na Wimbo bora wa mwaka.
Kwa upande wa Filamu vipengele vitakavyoshindaniwa ni Filamu bora ya Mwaka, Muigizaji Bora wa Kiume na Muigizaji Bora wa kike.
Tuzo za EATV 2016 zinafanyika kwa udhamini wa Coca Cola na Vodacom Tanzania .