Ole Gunnar amchapa Sir Ferguson

Jumatatu , 8th Mar , 2021

Baada ya klabu ya Manchester United kuibuka na ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Manchester City jana Machi 7, 2021 kwenye dimba la Etihad, sasa Ole Gunnar Solskjær ameweka rekodi ambayo hata kocha wa heshima wa timu hiyo Sir Alex Ferguson hakuiweka.

Ole Gunnar Solskjær na Sir Alex Ferguson

Solskjær sasa ndio kocha wa kwanza katika historia ya Manchester United kushinda mechi zake tatu mfululizo za kwanza, akiwa kama kocha nyumbani kwa wapinzani wao Manchester City, uwanja wa Etihad. 

Si hilo tu lakini pia ushindi huo ambao magoli yake yalifungwa na Bruno Fernandes dakika ya 2 ya mchezo kwa mkwaju wa penati pamoja na Luke Show dakika ya 50, umemfanya Ole Gunnar kuwa kocha wa kwanza katika makocha 67 ambao Guardiola amekutana nao kumfunga mara 4 mhispania huyo, ikiwa ni mara nyingi zaidi kuliko alivyopoteza kwa makocha wengine.

Pep Guardiola (kushoto) na Ole Gunnar Solskjær

Pia Manchester City rekodi yao ya kutofungwa katika michezo 28 imekoma baada ya kipigo hicho. Ikumbukwe Manchester City walikuwa hawajafungwa kwenye michuano yote tangu Novemba 2020 walipopoteza 0-2 dhidi ya Tottenham Hotspurs.

Machi 7, 2021 imeingia kwenye kitabu cha rekodi ikiwa ni siku ya pili kwa Manchester City na Liverpool kufungwa katika siku moja baada ya Liverpool nao kufungwa 1-0 na Fulham. Mara ya mwisho timu hizi mbili kufungwa siku moja ilikuwa ni Machi 3, 2017 ambapo Liverpool ilifungwa na Manchester United huku Manchester City ikifungwa na Wigan Athletics.