Jumatano , 22nd Nov , 2017

Kocha wa klabu ya soka ya Lipuli FC Suleiman Matola amejinadi kuwa kikosi chake ndio kitakuwa timu ya kwanza kuwafunga vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara Simba SC.

Lipuli FC itasafiri kutoka Iringa hadi jijini Dar es salaam kucheza na Simba kwenye mchezo wa raundi ya 11 utakaopigwa jumapili kwenye uwanja wa Chamazi.

“Tumejipanga vyema na naamini sisi ndio tutakuwa timu ya kwanza kuifunga Simba, tunaamini Simba wanakikosi bora lakini tutawashangaza mashabiki wa soka Tanzania”, amesema Matola.

Matola ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba akiwa pia amewahi kufundisha kikosi cha pili cha timu hiyo ameongeza kuwa, kikosi chake kina wachezaji wanaoweza kuizuia Simba isifunge bao na wao kufunga na kuondoka na alama tatu.

Lipuli ambayo imepanda daraja msimu huu inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 13 ikizidiwa alama nane na Simba ambayo inaongoza msimamo huo.