Jumanne , 22nd Oct , 2019

Muimbaji wa nyimbo za Injili hapa nchini, Joel Lwaga, ameeleza sababu ya waimbaji wa nyimbo za Injili kwa sasa kutotaja neno Yesu kwenye nyimbo zao, japokuwa lengo kubwa ni kumfanya Yesu awe maarufu miongoni mwa wanaomuamini.

 

Lwaga ametoa kauli hiyo, wakati akizungumza kwenye kipindi cha Kikaangoni, kinachorushwa kupitia kurasa za Facebook na Youtube ya East Africa  TV.

"Suala la kutaja jina la Yesu kwenye baadhi ya nyimbo, mimi huwa nataja, unajua maana ya Injili ni habari njema kutoka kwa Yesu na kumfanya  Yesu kuwa maarufu kwenye maisha ya watu, ila kwa upande wangu naimba kile ambacho  roho mtakatifu amenijalia kuimba, hata kama ikitokea haia neno Yesu." amesema Lwaga.

"Kwa mfano sitabaki nilivyo ule ujumbe ni wa kiinabii kabisa nilioneshwa na Mungu, japokuwa wimbo mwanzo mpaka mwisho hakuna neno Yesu, kwa sababu huwa nakuwaga na  ufunuo zaidi ndiyo huwa naweka neno Yesu." ameongeza Joel Lwaga.

Aidha Joel Lwaga amesema, kwenye masuala ya siasa kwa sasa anavutiwa zaidi na Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, kutokana na mambo makubwa anayoyafanya.