Ijumaa , 23rd Mei , 2014

Wakazi wanaoishi karibu na soko la Mapinduzi Mwananyamala jijini Dar es Salaam, wameelezea hofu ya uwezekano wa kuugua ugonjwa wa homa ya Dengu, kufuatia mazingira machafu katika soko hilo ambalo linatumiwa na idadi kubwa wakazi wa mwananyamala.

Maeneo machafu na yenye maji yaliyotuama kama haya ni kivutio pamoja na mazalia mazuri ya mbu wanaoeneza homa ya Dengue.

Wakizungumza na East Africa Radio katika eneo la soko hilo, wakazi hao wamesema licha ya halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kufahamu hali hiyo lakini hakuna jitihada za kuhakikisha mazingira ya soko hilo yanafanyiwa usafi.

Akizungumzia hali hiyo Mwenyekiti wa soko la Mapinduzi Bw. Hamisi Marande amesema wameshatoa taarifa kwa halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni lakini halmashauri haikuchukua hatua zozote na hivyo wafanyabiashara katika soko hilo kulazimika kufanya biashara zao kwenye hali ya wasiwasi.