Jumatatu , 25th Aug , 2014

Wanawake wajasiriamali nchini Tanzania, wametakiwa kujiunga katika Jumuiya na taasisi za wajasiriamali wanawake, ili kuwapa uwezo, ujuzi, mbinu pamoja na maarifa ya kuuza bidhaa zao katika masoko ya kimataifa yakiwemo masoko ya kikanda.

Bi. Suzan Mtui, Mtendaji Mkuu wa Chemba ya wafanyabiashara wanawake nchini Tanzania ya Tanzania Women Chamber of Commerce - TWCC.

Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam leo na Mtendaji Mkuu wa Chemba ya wafanyabiashara wanawake ya Tanzania Women Chamber of Commerce Bi. Suzan Mtui, wakati wa mkutano wa pamoja wa wenyeviti wa taasisi na mashirika yote tisa yanayounda chemba ya wafanyabiashara wanawake nchini.

Mkutano huo umeitishwa kwa ufadhili wa taasisi ya wanawake ya Umoja wa Mataifa ya UN Women ambapo washiriki kutoka ofisi zote za kanda na TWCC, wanakutana kwa siku mbili kwa ajili ya kujadili kwa pamoja katiba za kila taasisi, ili kuwa na mwongozo wa pamoja wa namna ambavyo wajasiriamali wanawake nchini wanavyoweza kujumuika kukuza shughuli za kiuchumi na ujasimali baina yao.

Akizungumza katika mkutano huo, Bi. Suzan ametaja changamoto kadhaa zinazowakabili wanawake wajasiriamali hasa wanapokwenda kuuza biashara zao katika masoko yaliyopo nje ya Tanzania kuwa ni pamoja na mbinu chafu zinazotumiwa na wafanyabiashara wa nchi husika hasa lugha za kigeni ambazo wajasiriamali wanawake kutika nchini wamekuwa hawana uelewa nazo.

Ametolea mfano wa nchi ambazo wajasiriamali wamekuwa wakipata shida kuwa ni Msumbiji ambako wakati mwingine wapinzani wao wamekuwa wakizungumza Kireno, Rwanda na Burundi ambako huzungumzwa Kifaransa na Kibelgiji na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako wajasiriamali kutoka nchini hukutana na kikwazo cha lugha ya Kifaransa.

Bi. Suzan amesema mikakati ipo mbioni kuhakikisha wajasiriamali wanawake wanaanza kufundishwa lugha adimu kama Kifaransa, Kireno na Kiingereza, ili kuwapa uwezo wa kumudu mazingira shindani ya kibiashara, hatua aliyosema kuwa itasaidia kuongeza masoko ya bidhaa zinazouzwa na kuzalishwa na wanawake wa hapa nchini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TWCC Bi. Fatma Riyami amesema wanawake nchini wana ari pamoja na uwezo wa kuuza bidhaa zao katika masoko ya kikanda likiwemo soko la pamoja kwa nchi za Afrika Mashariki na kwamba kinachohitajika ni mikakati ya kuwajengea uwezo mara kwa mara wa namna wanavyoweza kupenyeza bidhaa zao katika masoko husika hasa kutokana na mbinu za biashara nazo kubadilika kila wakati.

Aidha, Bi. Riyami amewashauri wajasiriamali wanawake wa hapa nchini kuboresha ubora na muonekano wa vifungashio vya bidhaa zao kwa maelezo kwamba vifungashio duni ni moja ya vyanzo vya kukosekana kwa soko licha ya bidhaa husika kuwa na viwango vinavyostahili na kuhitajika katika soko.

Chemba ya wajasiriamali wanawake ilianzishwa mwaka 2005, ikiwa na vyama wakilishi vinane pamoja na makampuni Themanini na Tano ambayo kwa pamoja yamewakutanisha wanawake wanaojishughulisha na ujasiriamali kutoka katika fani za usindikaji vyakula, biashara ya kushona na kuuza nguo, bidhaa za kazi za mikono pamoja na utoaji huduma.

Wanawake wengine ni wale wanaouza bidhaa za madini na vito, usafi na huduma katika maofisi, utalii, ujengaji uwezo wanawake pamoja na kilimo.