Jumatano , 30th Mar , 2016

Huduma za matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Mtwara, Ligula, zilikosekana kwa muda jana baada ya madaktari na wauguzi kugoma kwa kushinikiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwakamata watu wanaodaiwa kumpiga daktari wa hospitali hiyo.

Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu

Wakizungumza hospitalini hapo, baadhi ya wagonjwa wamesema kuwa toka wamewasili hakuna huduma yoyote ya matibabu iliyotolewa kwao zaidi ya kupokelewa mapokezi na kupatiwa cheti kisha kuambiwa wasubiri huku kukiwa hakuna dalili zozote za kuhudumiwa.

Wakizungumza mbele ya Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo wamesema kuwa hali ya usalama wao iko mashakani kutokana na kutokuwapo kwa ulinzi wa kutosha hospitalini hapo huku wengine wakipata vitisho kutoka kwa wananchi.

Akitoa tamkoa la Serikali juu ya tukio la kupigwa kwa daktari, Mhe. Ummy Mwalimu, amevitaka vyombo vya dola kutosita kuwachukulia hatua wananchi wote wanaokwenda kinyume na matakwa ya sheria ili kuwahakikishia watoa huduma za afya usalama na amani wakati wa kutekeleza wajibu wao.

Aidha, kamanda wa polisi Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Henry Mwaibambe, amesema watuhumiwa wawili wanaodaiwa kutekeleza tukio la kumpiga dkt. Dickson Sahini. hilo tayari wamekamatwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakani haraka.

Sauti ya Ummy mwalimu akizungumzia hatua za kuchukuliwa kwa kupiga Daktari