Jumanne , 4th Nov , 2014

Tanzania kesho itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa kuhusu uwekezaji, ambapo takribani wawekezaji Hamsini wenye mtaji mkubwa wa pesa watakutana na Watanzania ambao ni wamiliki wa makampuni yanayotafuta pesa kwa ajili ya uwekezaji.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Tanzania Dkt Godfrey Simbeye.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Tanzania – TPSF, Dkt Godfrey Simbeye, amesema hayo jijini Dar es Salaam leo, na kufafanua kuwa mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya TPSF ya kuanzisha mfumo wa mitaji ya ubia kwa ajili ya kukuza fursa za uwekezaji.

Kwa mujibu wa Dkt Simbeye, wawekezaji hao wana mtaji wa fedha zinazozidi shilingi za Kitanzania Trilioni Themanini, ambazo watakuwa tayari kuzitoa kwa miradi iliyobuniwa na wafanyabiashara wa Kitanzania, kupitia utaratibu wa miradi ya ubia baina ya wawekezaji hao na wale wa ndani.

Dkt Simbeye amesema hii ndiyo fursa pekee kwa wafanyabiashara wa Tanzania waliokuwa wanatafuta mikopo ya kufadhili biashara zao, kuchangamkia fursa ya kukutana na wafanyabiashara wanaoutafuta mahali pa kukopesha fedha zao.

Mkurugenzi huyo wa TPSF ameongeza kuwa hii ndiyo nafasi ya watanzania wenye ndoto ya kuanzisha miradi mikubwa ikiwemo viwanda vya magari na ambao walikuwa hawajui wapi watapata kiasi kikubwa cha pesa za kugharamia miradi yao.