Jumatano , 6th Jul , 2016

Mgogoro uliokuwa unakikabili kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichopo jijini Dar es Salaam umemalizika baada ya ofisi ya Msajili wa Hazina kufanya mabadiliko ya uongozi kiwandani hapo na kufanya uzalishaji kuendelea kama ilivyokuwa hapo awali.

Mgogoro huo ni pamoja na ukiukwaji wa sheria za kazi, kushuka kwa ufanisi, malimbikizo ya mishahara pamoja na madai ya ukiukwaji wa sheria na mikataba ya ubia katika ubinafsishaji wa kiwanda hicho.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Gerard Chami, ameiambia East Africa Television kuwa masuala hayo yameanza kupatiwa ufumbuzi na hivyo kumaliza migomo ya muda mrefu iliyokuwa inakikabili kiwanda hicho.

"Tunapenda kuutaarifu umma kuwa mgogoro uliokuwa unakikabili kiwanda cha Urafiki umekwisha na sasa shughuli za uzalishaji kiwandani pale zinaendelea kama kawaida," amesema Chami.

Kwa mujibu wa Msemaji huyo wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, chanzo cha matatizo yote yaliyokuwa yanakikabili kiwanda hicho ni pamoja na safu mbovu ya uongozi iliyokuwa inaundswa na wazawa, ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa inakwamisha utendaji wa kila siku wa kiwanda na hivyo kusababisha kushuka kwa ufanisi na migogoro isiyo ya lazima.

Katika hatua nyingine, Chami amesema hivi karibuni ofisi ya Msajili wa Hazina itatoa taarifa rasmi kuhusiana na zoezi la uhakiki wa viwanda, makampuni na mashamba yaliyobinafsishwa kujua iwapo waliokabidhiwa wanayaendeleza kwa mujibu wa mikataba na hatua ambazo serikali itazichukua.

"Tunawaomba wananchi wawe wavumilivu wakati tunapofanya mapitio ya ripoti ya uhakiki wa makampuni yaliyobinafsishwa kwani upembuzi wake unahitaji umakini wa hali ya juu ili kuepuka uonevu ambao wakati mwingine unaweza kusababisha serikali ifikishwe mahakamani,"