Mbunge ataja sababu za Magufuli kuongezewa muda

Alhamisi , 4th Feb , 2021

Mbunge wa Makambako kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Deo Sanga, amewataka wabunge wenzake kumuongezea muda Rais Magufuli, kwa kuwa amefanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kwamba asipotaka wabunge wamlazimishe.

Kushoto ni mbunge wa Makambako, Deo Sanga na kulia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli

Kauli hiyo ameitoa Bungeni Dodoma, wakati wa kikao cha pili mkutano wa pili wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema kuwa kuna watu ukiwaongezea muda ni adhabu, lakini Rais Dkt. Magufuli, anastahili kuongezewa ili ayakamilishe aliyoyaanzisha.

"Rais wetu amefanya kazi kubwa, ombi langu hapa ndani atake asitake tumuongezee muda ili aweze kufanya kazi yake vizuri ili mipango aliyoipanga ikamilike, atake asitake tumlazimishe, nilisema kipindi fulani hata China walifanya hivyo si dhambi kwa mtu anayefanya vizuri hata nyie wabunge mliorudi maana yake mlifanya vizuri ndiyo maana watu walisema tena mrudi", amesema Mbunge Sanga

Akitoa hoja yake katika ombi hilo, Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, alisema kuwa kila mtu anaujua msimamo wa Rais Magufuli, kwamba hataongeza muda lakini maoni ya mbunge hayazuiliwi kuzungumza kile anachoona.