Jumapili , 20th Aug , 2017

Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Temeke limemuomba Rais Dkt John Pombe Magufuli kuingilia kumaliza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 unaohusu umiliki wa kiwanja kilichopo Kitalu D Mtaa wa Everest jirani na Hospitali ya wilaya ya Temeke.

Mdhamini wa Kanisa la EAGT nchini Mchungaji Christom Isack Ngowi ametoa kauli hiyo kufuatia notisi inayowataka kuhamisha mali zote za kanisa kabla ya kesho Agosti 21, siku ambayo Manispaa ya Temeke imepanga kubomoa eneo hilo, kitendo ambacho waumini na viongozi wa kanisa hilo wamesema kingesubiri maamuzi ya barua waliyomuandikia Rais Magufuli kuhusu mgogoro huo.

Katika maelezo yao, viongozi na waumini wa kanisa hilo wameshangazwa na kile walichoeleza kuwa ni kutotekelezwa kwa maagizo ya mawaziri wa zamani wa ardhi akiwemo marehemu Mustafa Nyang'anyi na mwenzake Marcel Bujiku Komanya, ambao katika nyakati tofauti walizitaka mamlaka kulipatia kanisa la EAGT Temeke umiliki wa eneo hilo.

Kiwanja hicho kinagombewa kati yao na mfanyabiashara mmoja wa eneo hilo.