Jumanne , 2nd Aug , 2016

Mfuko wa kuendeleza sekta ya fedha nchini FSDT umesema unakusudia kufanya utafiti kuhusu upatikanaji wa huduma za kifedha, utafiti utakaohusisha pia athari za kiuchumi zinazotokana na maboresho yaliyofanywa kwenye Sheria ya Ongezeko la Thamani VAT.

Mkurugenzi Mkuu wa FSDT Sosthenes Kewe (wa kwanza kulia) akiwa na Gavana wa Benki Kuu katika moja ya shughuli zilizofanywa na taasisi hiyo hivi karibuni.

Mkurugenzi Mkuu wa FSDT Sosthenes Kewe, amesema hayo jijini Dar es Salaam leo, muda mfupi baada ya kushiriki hafla ya kuhitimishwa kwa shindano la ushiriki wa wanafunzi elimu ya juu katika masuala ya uwekezaji ambapo amesema utafiti huo utafanywa chini ya mradi ujulikanao kama FinScope.

“Sheria tayari imeshapitishwa na hakuna anayetaka kupingana na maagizo ya serikali …..ila kuna kila chembe ya ukweli kwamba sheria hii italeta madhara kwa watumiaji wa huduma za kibenki,” amesema Bw. Kewe.

Amesema kwa kufahamu hilo ndio maana katika utafiti wao wa Finscope mwaka huu, moja ya maeneo yatakayofanyiwa utafiti ni pamoja na athari zitokanazo na sheria mbali mbali za kodi ikiwemo hii inayolalamikiwa na wananchi wengi na kwamba kama sheria hiyo itaonekana ina madhara basi watatoa ushauri wao wa nini kifanyike.

Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Bw. Moremi Marwa yeye amesema elimu na ujuzi wa masuala ya uwekezaji ni muhimu ambapo ameishauri serikali kuangalia muundo mpya wa ubinafsishaji kwa kuyaandikisha mashirika hayo katika soko la hisa badala ya kuyauza kama ilivyofanyika miaka ya nyuma.

“Tunafurahi kuona idadi ya vijana wenye ujuzi na utaalamu wa uwekezaji imekuwa ikiongezeka lakini kinachohitajika ni kuwepo kwa mipango itakayoongeza ushiriki wa vijana hawa katika masoko ya mitaji na dhamana,” amesema Bw. Marwa.

Alipoulizwa juu ya mbinu za kuongeza uchangamfu wa kibiashara katika soko la hisa la Dar es Salaam; Bw. Marwa amesema “Mbinu pekee na ambayo inafaa kwa sasa ni kuongeza ushiriki wa mashirika ya umma katika soko hilo......tayari kuna ushahidi wa jinsi makampuni ya umma yaliyosajiliwa katika soko hilo yanavyofanya vizuri”

“Kinachotakiwa ni kwamba iwapo kutakuwa na ubinafsishaji mwingine siku za usoni basi ubinfsishaji huo ufanyike kupitia soko la hisa ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika kumiliki na kusimamia rasilimali zao,”