Jumanne , 12th Jan , 2021

Katibu wa kwanza wa vijana wa Afro Shirazi, Baraka Shamte, amesema kuwa siku ya mapinduzi Rais wa Zanzibar wa wakati huo, Hayati Abeid Karume, aliondoka Zanzibar na kukimbilia Bara ikiwa ni tahadhari ya kuepuka kukamatwa endapo utawala wa wakoloni ungeshinda.

Katibu wa kwanza wa vijana wa Afro Shirazi, Baraka Shamte.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 12, 2021, kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio, ikiwa leo Zanzibar inaadhimisha miaka 57 ya Mapinduzi, na kuongeza kuwa kamati ya mapinduzi iliongozwa na watu 14.

"Tarehe ile ya mapinduzi mchana wake Mzee Karume aliondoka Zanzibar akaja Bara kumfuata Nyerere na Kawawa, alisafiri kwa njia ya mtumbwi kukimbia yale mapinduzi, kwa tukahofia tukishindwa Mzee Karume anaweza akakamatwa, tukamshauri aje Bara, usiku ule alivyokuwepo huku Bara sisi tukafanya mapinduzi na ilivyofika Alfajiri tukawa tumeikamata nchi", amesimulia Mzee Shamte.

Aidha Mzee Shamte ameongeza kuwa, "Tulifanikisha mapinduzi baada ya kuundwa kamati maalum ya viongozi kwa kushirikiana na John Okero, huyu ni mwananchi mganda ambaye alihamia Zanzibar na kukaa kwa miaka mingi na hii kamati ndiyo iliyofanya mapinduzi".

Tazama video hapa chini