Jumapili , 26th Jul , 2015

Zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura jijini Dar es Salaam linaendelea huku bado likikabiliwa na upungufu wa mashine za BVR hali ambayo baadhi ya vijana wameanza kuitumia kama njia ya kujipatia kipato.

Zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura jijini Dar es Salaam linaendelea huku bado likikabiliwa na upungufu wa mashine za BVR hali ambayo baadhi ya vijana wameanza kuitumia kama njia ya kujipatia kipato.

Hali hiyo imebainika katika kituo cha Makoko kwa Mkwawa, Kata ya Kisukuru mtaa wa Luhanga, ambapo baadhi ya vijana waliokesha kituoni wamekuwa wakiuza nafasi za kuweza kujiandikisha kwa kiasi cha shilingi 5,000 kwa zile za mbali na 10,000 kwa zile za karibu.

Mbali na kituo hicho hali pia hali imekuwa tata katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam kutokana na wingi wa watu waliojitokeza mwishoni mwa juma hii leo ili kupata fursa ya kujiandikisha kwa kuwa kesho ni siku ya kazi.

Wananchi wa Kata ya Mburahati Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania waliojitokeza leo kujiandikisha katika daftari la kudumu la kupiga kura wameiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuongeza muda wa kujiandikisha, kutokana na kasoro zinazojitokeza mara kwa mara zikiwemo za mashine kushindwa kufanya kazi kwa wakati.

Wakizungumza na Kurasa leo, wananchi hao wakiwemo wazee wamesema licha ya tume ya uchaguzi kuagiza wazee, wajawazito na wagonjwa kupewa kipaumbele katika kujiandikisha lakini hali imekuwa ni tofauti katika baadhi ya vituo vilivyopo katika kata hiyo kwani wazee wameonekana wakiwa wamekaa chini na kushindwa kujua wafanye nini.

Wamesema hakuna utaratibu mzuri kwa makundi maalum kama ilivyobainishwa na tume ya taifa ya uchaguzi na hivyo kuitaka serikali ya mkoa wa Dar es salaam kuingilia kati kwa kuiomba tume ya uchaguzi kuongeza muda kwa hofu kwamba huenda wananchi wengi wasiandikishwe.