Jumamosi , 7th Nov , 2015

Takribani watu 53 wamekufa katika jiji la Dar es salaam tangu kuanza kwa ugonjwa wa kipindupindu miezi mitatu iliyopita.

Mratibu wa magonjwa ya milipuko kutoka wizara y Afya na ustawi wa jamii Bi. Victoria Bura amesema hayo leo jijini Dar es salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoa tathmini ya ugonjwa huo.

Amesema kwa sasa wilaya ya Temeke ndio inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa kipinudupindu ambapo kuna wagonjwa 39, Ilala mgonjwa 1 na Kinondoni mgonjwa 1.

Wakati hali ikielezwa kuwa mbaya, mama lishe katika soko la samaki la Feri jijini humo wamelalamikia kukosekana kwa maji safi katika soko hilo na hivyo kulazimika kupikia kwa kutumia maji ya chumvi kufuatia kukatwa kwa maji kunakotokana na deni linalodaiwa na kampuni ya maji safi na maji taka DAWASCO.

Kufuatia hali hiyo mama lishe hao wamesema sasa wamekuwa wakilazimika kununua maji kwa shilingi elfu moja hadi elfu mbili kwa dumu moja la lita ishirini huku wakieleza kukosekana kwa uhakika wa usalama wa vyakula vinavyopikwa kwa kutumia maji ya chumvi.

Wakati huohuo baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam wameelezea kusikitishwa kwao na tatizo la mara kwa mara la utiririshaji wa maji taka unaotokana na chemba ya maji taka katika barabara ya Upanga.

Wakieongea na KURASA leo wakazi hao wamesema tatizo hilo linatokana na kutokuwa na mipango endelevu ya mfumo wa maji taka na hivyo kuzidiwa kwa chemba hiyo kunakotokana na ongezeko la idadi ya watu katika jiji la Dar es salaam.

Baadhi ya mama lishe katika soko la feri
Baadhi ya mama lishe katika soko la feri