Mwenyekiti wa Jukwaa la Tiba Asili nchini Boniventura Mwalongo amesema hayo jijini Dar es Salaam leo na kufafanua kuwa hali hiyo inachangiwa na mgawanyiko mkubwa baina ya wadau wa tiba asili pamoja na vyombo vya dola, hususani vile vilivyopewa jukumu la kusimamia sekta ya tiba asili nchini.
Kwa upande wake, mjumbe wa Jukwaa hilo Bw. Mohamed Said Mangosongo amewasihi wanahabari nchini kushirikiana na vyombo vya dola katika kuwafichua watu wanaojihusisha na ramli chonganishi pamoja na matendo mengine maovu yanayochangia ukatili na mauaji kwa watu wenye ulemavu wa ngozi.
Akifafanua kuhusu mgawanyiko huo, Mwalongo amesema unahusisha zaidi vyombo vya maamuzi kuhusu nani anahusika kuingia katika baraza la tiba asili lililo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako tayari kuna fununu kwamba baadhi ya watu wasio na sifa na wanaotajwa kuwa wanajihusisha na upigaji ramli wameteuliwa kuwa sehemu ya wajumbe wa baraza hilo.
Mgawanyiko mwingine kwa mujibu wa Mwalongo ni pamoja na kutokuwepo kwa ushirikiano wa vyombo vya dola, ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa havishirikiani na wadau wa tiba asili hasa jinsi ya kuwabaini watu wanaojihusisha na ramli chonganishi.
Mzee Mangosongo kwa upande wake amesema iwapo kutakuwa na ushirikishwaji mzuri wa wadau, watoa tiba asili nchini watakuwa na msaada mkubwa wa kuwatambua watu wanaotumia jina la tiba asili kama kivuli cha wao kutenda maovu ikiwemo ukatili na mauaji kwa watu wenye ulemavu wa ngozi - Albino.