Saturday , 25th Apr , 2015

Mbunge wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe, Mh. Deo Filikunjombe amesikitishwa na kitendo cha diwani wa kata ya Luilo wilayani humo, Bw. Mathew Kongo kwa kitendo cha kuwashinikiza wananchi wasishiriki shughuli za maendeleo.

Mbunge wa jimbo la Ludewa mkoani Njombe, Mh. Deo Filikunjombe.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lifua na Luilo katika kata ya Luilo wilayani Ludewa, Mh. Filikunjombe amesema baadhi ya viongozi wanakichafua Chama Cha Mapinduzi kwa kupandikiza chuki kwa wananchi kwa makusudi na kwa manufaa yao binafsi jambo ambalo amedai kamwe hatalifumbia macho.

Katika kata ya Luilo, Mh. Filikunjombe akakerwa na kitendo cha diwani wa kata hiyo, bw, Mathew Mkongo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa, kuwashawishi wananchi wasishiriki kuchimba mashimo kwa ajili ya kusimika nguzo za umeme na kukwamisha jitihada zake na serikali kufikisha umeme kwa wananchi kwa mandeleo yao huku akitishia kumcharaza viboko hadharani.

Hata hivyo baadhi ya wananchi na viongozi akiwemo mtendaji wa kata hiyo ya Luilo, bw. Bosco Henjewele akawaomba radhi wananchi kuingizwa kwenye kasumba hiyo ya diwani wao na kwamba atakuwa bega kwa bega na wananchi kufanikisha zoezi la kufikisha umeme katika kata hiyo kwa manufaa ya wananchi.

Akizungumza kwa njia ya simu diwani huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri wilaya ya Ludewa, bw, Mathew Kongo amedai kwamba kazi ya kuchimba mshimo kwa ajili ya kusimika nguzo hizo za umeme sio kazi ya wananchi bali ni kazi ya TANESCO.