Mkuu wa Mkoa wa Arusha Daudi Ntibenda.
Changamoto inayotolewa ni kwa taasisi za kiserikali zinazojihusisha na utalii zikiwemo Bodi ya Utalii Tanzania, Shirika la hifadhi za wanyama nchini, Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro pamoja na Wizara yenyewe ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inatoa matangazo na majarida mbalimbali katika nchi za bara la Ulaya, Asia na Marekani ili kuwavutia wageni wengi zaidi.
Katika Mkutano wa kumi na sita wa chama cha waongoza watalii nchini TTGS,unaofanyika Jijini Arusha, Wadau wa Sekta hiyo pia wameitaka Serikali kuhakikisha inaboresha huduma zake katika viwanja vya ndege pamoja na kuondoa vikwazo vyote hususani vya barabarani ambavyo vimekuwa kero kwa wageni.
Akizungumza na wanachama hao, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Daudi Ntibenda ametoa mwito kwa wadau hao wa utalii kuhakikisha wanaimarisha uzalendo kwa kutoa taarifa za wageni wanaoonekana kuingia nchini wakiwa na malengo tofauti yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Aidha kwa baadhi ya watendaji katika chama cha waongoza watalii akiwemo mwenyekiti wake Sadock Johnson pamoja naye Haji Mbuguni wamesema shauku yao ni kuona serikali inachukulia kwa umakini mapendekezo yanayotolewa na chama hicho kutokana na wao kuwa kiungo muhimu kwa muda wote ambao wageni wanafanya shughuli za kitalii katika hifadhi mbalimbali nchini.
Zaidi ya waongoza watalii elfu mbili nchini kote wanatajwa kuwa wanachama wa TTGS, chama ambacho kinatajwa kuwa muhimu kutokana na watendaji wake kuwa katika nafasi nzuri ya kukuza na kuimarisha biashara ya utalii Tanzania.