Friday , 2nd Jan , 2026

Mabwawa ya maji yatakuwa ni suluhisho la kudumu ya mafuriko katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro.

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amezungumza na wakazi wa Tindiga wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro walioathirika na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Dkt. Mwigulu amezungumza hayo leo Januari 02, 2026 na amewaeleza wakazi hao kuwa Serikali inaendelea na mikakati ya kukabiliana na athari za mvua katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa Mabwawa eneo la Kidete.

Amesema kuwa ujenzi wa mabwawa hayo ya maji yatakuwa ni suluhisho la kudumu ya mafuriko katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro.

Ameongeza kuwa kwa sasa mpango huo upo katika hatua za kitalaam ikiwemo kumpata mkandarasi. ”Fedha imepatikana kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa kwa sasa tunaendelea na taratibu za kitaalam, Wizara zinazohusika hakikisheni mnakamilisha taratibu hizo ili ujenzi uanze”.

Aidha, akiwa ziarani mkoani Morogoro, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuelewa na kuthamini maamuzi ya kiserikali yanayolenga kulinda usalama wa raia, wakati akiwelezea sababu za kuahirisha safari za usafiri wa kisasa kama treni ya SGR kutokana na changamoto za hali ya hewa akisema ni jambo la kawaida na la kitalaamu duniani kote.

Amesema kuwa nchi zilizoendelea zenye teknolojia kama ya Tanzania hufanya maamuzi kama hayo pindi kunapotokea barafu au mvua za upepo zinazoweza kuathiri mifumo ya umeme na usalama wa abiria.

Kauli hii imekuja kufuatia hatua ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kusitisha kwa muda safari za treni za Standard Gauge Railway (SGR) kati ya Morogoro na Dodoma kuanzia Desemba 31, 2025 mara baada ya mvua kubwa kusababisha uharibifu wa miundombinu katika maeneo ya Kidete na Godegode.