Thursday , 25th Dec , 2025

JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga linamshikilia Mkazi wa Welei wilayani Lushoto mkoani Tanga Isaka Clement Ngulizi kwa kosa la kumshambulia na kumkata vidole vitatu mwanafunzi wa darasa la nne mwenye umri wa miaka kumi na moja (11).

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Almachius Muchunguzi amesema kwamba tukio hilo lilitokea Desemba 2 mwaka huu ambapo mtuhumiwa huyo alitekeleza ukatili huo kwa kisingizio cha kumkuta mtoto huyo akijaribu kuiba ndani ya nyumba yake.

Kamanda Muchunguzi ameyataja matukio mengine ya ukatili dhidi ya watoto ambayo Jeshi hilo limepata mafanikio makubwa katika kuyashughulikia mkoani humo likiwemo lile la Oktoba 8 mwaka huu katika Kijiji cha Kiloza wilayani Korogwe ambapo mmoja wa mtoto mwenye umri wa miaka mitatu (03) alijeruhiwa vibaya kwa kukatwa mguu wa kulia na kitu chenye makali.

Mtuhumiwa aliyemjeruhi vibaya mtoto huyo ni Abraham Yonathani ambaye uchunguzi ulibaini kuwa alifanya ukatili huo kutokana na wivu wa mapenzi.

Alieleza kwamba kufuatia ushahidi uliokusanywa na kuwasilishwa mahakamani Novemba 19 mwaka huu mtuhumiwa huyo alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka (07) Gerezani pamoja na kupewa amri ya kulipa fidia ya Sh.100, 000 kwa madhara.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa jamii hususani wazazi na walezi kuongeza umakini na ulinzi kwa watoto wadogo hususani katika kipindi cha sikukuu kwani baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa na tabia ya kuwaacha watoto kwenda kutembea peke yao bila uangalizi wa mtu mzima kwenye akili timamu.

Aidha, limetoa onyo kali kwa watu wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai na hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika mbele ya sheria kwa kumfanyia mtu mwingine ukatili.