Monday , 20th Oct , 2025

Huenda Klopp hajawahi kusema hivi moja kwa moja, kauli zake kwenye mahojiano na Steven Bartlett (DOAC) zinatoa picha kwamba wamiliki wa Liverpool, Fenway Sports Group (FSG), hawakumtendea haki.

Katika mahojiano hayo, Klopp alieleza uzito wa majukumu aliyokuwa nayo: “Kwenye upande wa maamuzi, kila kitu kilikuwa chini yangu. Richard Hughes na Michael Edwards walikuja baada ya mimi kuondoka, na si kwa sababu tulikuwa na mikwaruzano. Walihitaji viongozi ambao watafanya kazi kwa ukaribu na kocha mpya, Arne Slot. Lakini katika kipindi changu, hawakuwepo; maamuzi yote yalitoka kwangu, na wakati huohuo tulikuwa na jukumu la kushinda michezo yote.”

Uchambuzi:

FSG walimkosea sana Klopp. Inashangaza kwa nini waliruhusu majukumu yote ya timu kuwa juu yake wakati jukumu lake kuu lilikuwa ni kuiongoza timu kupata matokeo uwanjani.

Inaonekana ilikuwa rahisi kwa Arne Slot kuletewa wakurugenzi wa michezo na ufundi, jambo ambalo lingeweza kufanyika pia kwa Klopp. Kama FSG wangempa Klopp msaada wa kiuongozi kama huu, huenda angebaki kwenye klabu.

Taarifa za Ziada:

• Richard Hughes: Mkurugenzi wa Michezo wa Liverpool.

• Michael Edwards: Mtendaji Mkuu wa Uendeshaji wa Soka. Awali alikuwa mkurugenzi wa michezo lakini aliondoka baada ya kutofautiana na Klopp, na akarejea baada ya Klopp kuondoka.

• Fenway Sports Group (FSG): Kampuni inayomiliki asilimia kubwa ya hisa za Klabu ya Liverpool, inayoongozwa na John W. Henry.