
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imetangaza kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi kutoka Shilingi 275,060 hadi Shilingi 358,322, ikiwa ni ongezeko la asilimia 33.4.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, na kuongeza kuwa ongezeko hilo kwa sekta binafsi ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria.
Waziri Ridhiwani ameongeza kuwa Serikali inataka waajiri wote wa sekta binafsi kuhakikisha wanazingatia na kutekeleza kima hicho kipya cha mshahara kwa mujibu wa sheria na kuonya kuwa Ofisi yake haitasita kuchukua hatua kwa waajiri watakaokaidi au kushindwa kutekeleza agizo hilo kwa makusudi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake.
Kima hicho kipya cha mshahara kitaanza kutumika rasmi Januari 1, 2026, kikilenga kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kuleta uwiano na ongezeko la mishahara ya watumishi wa umma lililotangazwa awali. #EastAfricaTV