
Idara ya Uhamiaji imewaondoa nchini raia wawili wa kigeni kutoka nchini Ujerumani na Marekani baada ya kukiuka masharti ya viza zao za matembezi.
Kupitia taarifa yake kwa umma iliyoitoa leo, Oktoba 14 Idara hiyo imewataja raia hao kuwa ni Dkt. Brinkel Stefanie na Bi. Catherine Jannel Almquist Kinokfu na kuongeza kuwa wameondolewa nchini jana Oktoba 13, 2025.
“Tarehe 13 Oktoba, 2025 Idara ya Uhamiaji imewaondoa nchini raia wawili wa kigeni ambao ni Dkt. Brinkel Stefanie mwenye hati ya kusafiria ya Ujerumani namba C475MNGL na Bi. Catherine Jannel Almquist Kinokfu mwenye hati ya kusafiria ya Marekani namba A80321764 baada ya kubainika kuw wamekiuka masharti ya visa za matembezi”, imebainisha.
Kufuatia tukio hilo, Idara ya Uhamiaji imetoa wito kwa rai awa kigeni wanaoingia nchini kuishi kwa madhumuni mbalimbali kuzingatia matakwa yaliyoainishwa katika viza au vibali vya kusafiria kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Sura 54 pamoja na kanuni zake ili kuepuka usumbufu unaojitokeza wanapokiuka sheria.