Tuesday , 9th Sep , 2025

Nepal imeondoa marufuku ya mitandao ya kijamii baada ya kusababisha mapigano kati ya waandamanaji na polisi ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 19.

Maelfu ya vijana walikuwa wameingia kwa nguvu katika jengo la bunge katika mji mkuu Kathmandu jana Jumatatu, Septemba 8 wakiiomba serikali kuondoa marufuku yake ya mitandao 26 ya kijamii, zikiwemo Facebook na YouTube, na pia kuitaka kukabiliana na ufisadi.

Uamuzi wa kuondoa marufuku hiyo ulifanywa baada ya mkutano wa dharura wa baraza la mawaziri jana Jumatatu kushughulikia matakwa ya vijana hao maarufu kama Gen Z, Waziri wa Mawasiliano na Habari Prithvi Subba Gurung amesema katika taarifa. Zaidi ya watu 100 walijeruhiwa katika maandamano hayo, ambayo pia yalifanyika katika miji mingine nje ya mji mkuu.

Mitandao ya kijamii kama vile Instagram ina mamilioni ya watumiaji nchini Nepal, ambao wanaitegemea kwa burudani, habari na biashara. Serikali ilihalalisha marufuku yake, iliyotekelezwa wiki iliyopita, ili kukabiliana na habari ghushi, matamshi ya chuki na ulaghai mtandaoni.

Vijana walioingia mitaani jana Jumatatu walisema pia walikuwa wakipinga kile wanachokiona kuwa tabia ya kimabavu ya serikali. Wengi walishikilia mabango yenye kauli mbiu zikiwemo “Imetosha” na “mwisho wa rushwa”. Baadhi ya waandamanaji pia walirushia mawe nyumba ya Waziri Mkuu KP Sharma Oli katika mji wa Damak. Polisi mjini Kathmandu waliamua kutumia maji ya kuwasha, marungu na kufyatua risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji.

Wakati huohuo Waziri Mkuu KP Sharma Oli amesema amehuzunishwa sana na ghasia na idadi ya waathirika, akilaumu matukio ya siku hiyo kwa kujipenyeza kwa vikundi mbalimbali vyenye maslahi binafsi. Naye Waziri wa Mambo ya Ndani Ramesh Lekhak aliwasilisha kujiuzulu kwake jioni kufuatia ukosoaji mkubwa juu ya matumizi ya nguvu ya utawala wake wakati wa maandamano.

Wiki iliyopita, mamlaka iliamuru kuzuiwa kwa majukwaa 26 ya mitandao ya kijamii kwa kutozingatia makataa ya kujisajili na wizara ya mawasiliano na teknolojia ya habari ya Nepal. Serikali ya Nepal imeteta kuwa haipigi marufuku mitandao ya kijamii bali inajaribu kuhakikisha zinaendeshwa kulingana na sheria za Nepal.