Monday , 18th Aug , 2025

Leo rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anafanya  mkutano na rais wa Marekani Donald Trump huko Washington nchini Marekani.

Mkutano huu unakuja siku chache tu baada ya Trump kukutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi, uliofanyika jimbo la Alaska nchini Marekani.

Lakini Zelensky hatakuwa peke yake katika mkutano huo. Atasindikizwa na viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Finland, Kamisheni ya Ulaya na Nato.

Hatua ya viongozi hao wa nchi za Ulaya kuambatana na Zelensky si ya kawaida na si bahati mbaya pia. 
Wanalenga kutuma ujumbe mzito kwa Trump na serikali yake lakini pia kwa Putin.

Ni kweli Trump amefanya jitihada kubwa za kutaka kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine, lakini Zelensky na viongozi wa Ulaya wana wasiwasi kwamba amekuwa na huruma kwa Putin na kwamba anaweza kuingia katika mtego wa kumpa rais huyo wa Urusi kile anachokitaka.

Pamoja na kutaka hakikisho kwamba Ukraine haitajiunga na Nato, kutokuendelea kusaidiwa kijeshi na Ulaya na madai mengine, Putin anataka apewe maeneo kadhaa ya upande wa Mashariki ya Ukraine ambayo anadai kihistoria yalikuwa ni ya Urusi.

Lakini Ukraine na Ulaya inakataa matakwa hayo na kusema kumpa Putin hayo maeneo ili asimamishe vita ni sawa na kumzawadia mchokozi na mvamizi.

Kwa hivyo ujumbe wa kwanza wa Umoja wa Ulaya kuambatana na Zelensky ni kumwambia Trump; "Usimzawadie Putin kwa uchokozi alioufanya".

Ujumbe wa pili watakaoupeleka ni kwamba wanataka hakikisho la Marekani na wajibu wake katika kuhakikisha Putin hatavamia tena Ukraine muda mfupi baada ya kusitishwa kwa vita vinavyoendelea sasa.

Ujumbe mwingine wa muhimu ambao viongozi hao wa Ulaya na Zelensky wanatumaini kumpa Trump ni kwamba wanaitazama vita ya Urusi na Ukraine kuwa ni vita ya Ulaya.

Wao wanaamini kwamba Putin asipodhibitiwa vya kutosha basi hatoishia kuvamia Ukraine tu, bali ataendelea kuvamia nchi zingine pia za Ulaya, hasa zile zinazopakana na Urusi kama vile Poland, Finland na Estonia.