Monday , 18th Aug , 2025

Makumi ya watu wamekamatwa huku maelfu ya Waisraeli wakiingia mitaani siku ya jana Jumapili Agosti 17 katika maandamano ya nchi nzima.

Waandamanaji walidai kukomesha vita vya Israel huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka 50 waliosalia, ambapo takriban 20 wanaaminika kuwa bado wako hai. Pia walikusanyika katika maeneo ikiwa ni pamoja na nje ya nyumba za wanasiasa, makao makuu ya jeshi, na kufunga barabara kuu ambapo walinyunyiziwa mizinga ya maji na polisi.

Wakati maandamano hayo yakiendelea kote Israel, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alihutubia Baraza lake la Mawaziri la mrengo wa kulia akisema vita vitaendelea. Netanyahu alisema Hamas haitapokonywa silaha peke yake, lakini Israel ni lazima itekeleze upokonyaji silaha wa Gaza kwa kuchukua hatua mfululizo dhidi ya jaribio lolote la kigaidi la kumiliki silaha na kujipanga.

Pia Netanyahu alikosoa vitendo vyao akisema wito wao wa kumaliza vita bila kuwashinda Hamas, ni sawa na kufanya misimamo migumu ya kundi la wanamgambo kuendelea na kuchelewesha kuachiliwa kwa mateka.

"Pia wanahakikisha kwamba maafa ya tarehe 7 Oktoba yatajirudia tena na tena, na kwamba wana wetu na binti zetu watalazimika kupigana tena na tena katika vita visivyoisha," alisema.

Maandamano hayo yamekuja baada ya wiki kadhaa baada ya makundi ya wanamgambo kutoa video za mateka waliodhoofika na Israel kutangaza mipango ya kufanya mashambulizi mapya.