
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa nyumba za bei nafuu eneo la Kilimani, Nairobi, Ruto ameelezea masikitiko yake kuhusu kile alichokitaja kuwa ni hali ya kipekee ya vurugu na upinzani mkali dhidi ya serikali yake.
Alitilia shaka kwa nini viongozi wa upinzani wamekuwa wakionesha msimamo mkali dhidi yake tofauti na walivyofanya kwa marais waliomtangulia kama Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta.
Kwa mujibu wa Ruto, haieleweki ni kwa nini fujo na maandamano yanalengwa kwake binafsi, huku akisema kuwa si haki kuendeleza siasa za chuki, kiburi na ukabila.
Alisisitiza kuwa Wakenya wote ni sawa na hakuna aliye bora kuliko mwingine, akitoa wito wa mshikamano wa kitaifa.
Aidha Rais wa Kenya William Ruto ameweka wazi kuwa hataruhusu yeyote kujaribu kuipindua serikali kwa njia zisizofuata katiba.
Rais Ruto ameeleza kuwa kuwa nchi haitakubali kusambaratishwa na watu wachache wasiopenda utaratibu wa kidemokrasia, na kuongeza kuwa serikali yake itasimamia sheria kwa uthabiti.
Ruto pia amewataka viongozi wa upinzani waache siasa za vurugu na badala yake wajipange kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 kwa kuwasilisha sera na mipango yao kwa wananchi kwa njia ya amani na demokrasia.#