Thursday , 26th Jun , 2025

Spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson wakati wa Hotuba yake ya kuhitimisha Mkutano wa 19 wa Bunge la 12 la Tanzania leo Alhamisi Juni 26, 2025 ameliambia Bunge la Tanzania kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka minne ya Uongozi wake amelitendea haki Taifa kwa kuhakikisha maend

Spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson wakati wa Hotuba yake ya kuhitimisha Mkutano wa 19 wa Bunge la 12 la Tanzania leo Alhamisi Juni 26, 2025 ameliambia Bunge la Tanzania kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka minne ya Uongozi wake amelitendea haki Taifa kwa kuhakikisha maendeleo na mafanikio yanapatikana.

Dkt. Tulia ameyaeleza hayo, akitaja baadhi ya miradi mikubwa iliyotekelezwa kwa kipindi kifupi cha Uongozi wa Rais Samia, ikiwemo ujenzi wa Reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar Es Salaam, Morogoro hadi Dodoma, Ujenzi wa Daraja la JP Magufuli (Kigongo-Busisi) Mkoani Mwanza pamoja na mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere.

Akimtaja kama Kiongozi mahiri, shupavu na nwenye dira, Dkt. Tulia pia ametaja mafanikio ya miradi ya Ujenzi wa Hospitali za Mikoa, Hospitali za Rufaa za Mikoa pamoja na mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za Kijamii ikiwemo sekta ya elimu, Maji pamoja na usambazaji wa nishati ya umeme.

"Tumeona umeme ukifika kule kwenye Vijiji, tumeona umeme ukifika kwenye mitaa na lipo hili lililomletea sifa Dkt. Samia na kuliletea sifa Taifa letu. Dkt. Samia ni kinara wa nishati safi duniani."Amesema Spika Tulia Ackson.

Spika Tulia pia ametaja miradi mbalimbali iliyotekelezwa Jimboni kwake ikiwa ni pamoja na Mradi wa Maji Kiwira, Barabara ya Njia nne Mbeya Mjini, Hospitali ya Wilaya Igawilo pamoja na usambazaji wa umeme kwenye Kata 14 za pembezoni, akimshukuru Rais Samia na kumtakia kheri katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Mei 31, 2025 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilimtunuku tuzo maalum ya heshima ya kutambua mchango wa Dkt. Samia Suluhu Hassan  katika kulitumikia Taifa na kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwa ni miongoni mwa msururu mrefu wa tuzo na Shahada za Udaktari wa heshima alizopewa Dkt. Samia kutoka kwa Taasisi na Vyuo vya ndani na nje ya nchi.