Friday , 20th Jun , 2025

Hapo jana moja ya stori kubwa katika ulimwengu wa michezo ilikuwa ni rekodi iliyowekwa na klabu ya mpira wa kikapu ya Los Angeles Lakers inayoshiriki ligi ya mpira wa kikapu nchini Marekani NBA, ambapo imeweka rekodi ya kuwa timu pekee iliyonunuliwa kwa bei ghali zaidi duniani.

Lakers imeuzwa kwa pesa za marekani dola Bilioni 10 sawa na Trilioni 26 (26,420,439,543,706.00) za Tanzania, ambayo hii ni sawa na asilimia 53% ya bajeti ya Tanzania ya mwaka wa fedha uliopita  2024/2025 ambayo ilikuwa Trilioni 49, lakini pia thamani hii ya Lakers inakaribia sawa na nusu bajeti ya serikali ya Tanzania ya mwaka wa fedha 2025/26 ambayo ni Trilioni 56.

Tajiri aliyeinunua klabu hiyo ni Mark Walter, ambaye anakadiriwa kuwa na utajiri wenye thamani ya dola za marekani Bilioni 6.1 sawa na Trilioni 16 za Tanzania, huku katika orodha ya mabilionea duniani kulingana na mtandao wa Forbes (2025) Mark yupo nafasi ya 581.

Mbali na kuinunua klabu hiyo pia Mark ni CEO na mwanzilishi wa kampuni ya Guggenheim Partners yenye thamani zaidi ya $320–335 bilioni, na pia vilevile ana hisa za umiliki wa klabu mbali mbali ikiwemo Chelsea, Strasbourg FC ya ufaransa, Los Angeles Dodgers (MLB), Los Angeles Sparks (WNBA).