Saturday , 10th May , 2025

Mshambulizi wa Manchester City Erling Haaland yuko tayari kuwakabili  Southampton Jumamosi hii. Nyota huyo alikuwa nje ya uwanja tangu mwezi Machi baada ya kupata jeraha la kifundo cha mguu katika mechi ya Kombe la FA dhidi ya Bournemouth.

Erling Haaland - Mshambulizi wa Manchester City

Haaland raia wa Norway mwenye umri wa 24 amefunga magoli 21 EPL, tofauti ya magoli 7 dhidi ya kinara Mohamed Salah wa Liverpool mwenye magoli  28 huku nafasi ya pili inashikiliwa na Alexander Isak wa Newcastle United aliyefunga magoli 23. Imesalia michezo mitatu pekee kutamatika kwa msimu 2024/25 ambao tayari Liverpool wameshatangazwa kuwa mabingwa wa Ligi hiyo.

Kuelekea mchezo wa hapo kesho dhidi ya Southampton, Guardiola amesema "Haaland yuko tayari, yuko fiti. ila suala la kuanza kikosi cha kwanza, tutaona kesho.

City wako katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wakiwa na alama 64 ikiwa ni tofauti ya pointi tatu dhidi ya Nottingham Forest walio katika nafasi ya sita kwa alama 61, huku klabu zikipigania kupata moja ya nafasi tano za juu ambazo msimu ujao zitashiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.