Friday , 4th Apr , 2025

Mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya kujihami ya NATO wanakutana mjini Brussels kwa siku mbili kujadiliana njia za kujiimarisha kwa kuzingatia umoja na usawa.

Mkutano huo unafanyika chini ya shinikizo kutoka Washington la kutaka nchi wanachama wengine wa NATO watoe mchango zaidi wa kifedha kwa kuongeza matumizi yao ya ulinzi hadi asilimia 5 ya pato la taifa.

Mawaziri hao wa mambo ya nje wa NATO walikubaliana kwamba nchi zote 32 wanachama wa muungano huo zinapaswa kuongeza juhudi katika kuongeza matumizi yao ya ulinzi hadi kufikia asilimia 5 ya pato la taifa. 

Kwa sasa, Poland pekee ndio inakaribia kiwango hicho kwa kuwa na asilimia 4,7, Marekani 3,4 huku mataifa kama Italia na Uhispania yakiwa chini ya asilimia moja. 

Nchi za Ulaya zimeahidi kufikia asilimia 5 mwaka ujao.

Baadhi ya wanadiplomasia mjini Brussels wamesema kwamba mkutano huo utaangazia pia suala la vita vya Ukraine ambapo mataifa ya Ulaya yamedhihirisha wazi wasiwasi wao kuhusu ukaribu unaoshuhudiwa sasa kati ya Marekani na Urusi ambayo ndio inachukuliwa kama kitisho kikuu kwa NATO.