
Wahudumu wa afya huko Gaza wamesema kuwa watu 23 wameuawa usiku wa kuamkia leo kufuatia mashambulizi ya Israel
Watoto watatu na wazazi wao ni miongoni mwa waliouawa walipokuwa kwenye hema lao karibu na mji wa kusini wa Khan Younis.
Hayo yameelezwa na madaktari wa hospitali ya Nasser, ambayo imepokea idadi kubwa ya maiti na watu waliojeruhiwa tangu Israel ilipoanzisha wiki iliyopita, wimbi jipya la mashambulizi makali ya mabomu huko Gaza.
Tangu kuanza kwa vita hivyo Oktoba 7 mwaka 2023 kufuatia uvamizi wa wanamgambo wa Hamas kusini mwa Israel, zaidi ya Wapalestina 50,000 wameuawa na wengine zaidi ya 113,000 wamejeruhiwa bila hata hivyo kutoa idadi kamili ya raia na wapiganaji.
Idadi hiyo ni kwa mujibu wa wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas. Israel kwa upande wake inadai kuwa imefanikiwa kuwaangamiza wapiganaji 20,000.
Katika hatua nyingine, msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee amewataka wakazi wa miji ya kaskazini mwa Gaza ya Jabalia, Beit Lahia na Beit Hanoun kuondoka katika maeneo yao kufuatia mashambulizi kadhaa yaliyopangwa kufanyika eneo hilo, akisema hilo ni kutokana na kuwa makundi ya kigaidi kwa mara nyingine yameanzisha kurusha makombora kutoka maeneo yenye watu wengi huku akiwataka raia kuelekea mara moja katika maeneo ya kusini mwa Gaza.