Sunday , 23rd Mar , 2025

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Dkt. Charles Msonde amesema daraja la J.P Magufuli (Kigongo Busisi) lenye urefu wa KM 3 litaanza kutumika rasmi Aprili 30 mwaka huu.

Daraja la J.P Magufuli (Kigongo-Busisi)

Hata hivyo, amesema ifikapo Aprili 10, 2025 magari yataanza kupita upande mmoja kwenye daraja hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 97 huku ujenzi wake ukigharimu zaidi Shilingi ya bilioni 610.

Daraja hilo limejengwa kwa lengo la kuunganisha Barabara Kuu ya Usagara - Sengerema Geita KM90 ambayo ni sehemu ya barabara iliyopo kwenye Ushoroba wa Ziwa Victoria inayoanzia Sirari mpakani mwa Tanzania na Kenya hadi Mutukula mpakani mwa Tanzania na Uganda.

Kwa sasa sehemu ya barabara hiyo eneo la Kigongo Busisi inaunganishwa kwa kutumia vivuko vikubwa vitatu vya MV Mwanza, MV Misungwi na MV Sengerema.

Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 3 na upana wa meta 28.45 lina  njia mbili za magari zenye upana wa mita 7  kila upande.