Friday , 21st Mar , 2025

Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini agizo kuu la kuvunja Idara ya Elimu, kutimiza ahadi ya kampeni na lengo la muda mrefu la baadhi ya wahafidhina.

Akiishtumu idara hiyo kwa kushindwa kutoa huduma, rais Trump aliapa kurudisha pesa inazodhibiti kwa majimbo mahususi.

Trump alisema kuwa alisema kuwa ataifunga haraka iwezekanavyo idara hiyo ingawa Ikulu ya White House ilikiri kwamba kuifunga idara hiyo moja kutahitaji kuungwa mkono na mabunge ya Congress.

Hatua hiyo tayari inakabiliwa na changamoto za kisheria kutoka kwa wale wanaotaka kuzuia kufungwa kwa idara hiyo pamoja na kupunguzwa kwa wafanyakazi wake.

Akiwa amezungukwa na watoto walioketi kwenye madawati ya shule katika Ikulu ya White House Trump alisema Marekani inatumia pesa nyingi zaidi katika elimu kuliko nchi nyingine yoyote lakini aliongeza kuwa wanafunzi wanashika nafasi ya chini kabisa ya orodha hiyo.

Ikulu ya White House ilisema kuwa utawala wake utachukua hatua ya kukata sehemu za idara ambazo zimesalia ndani ya mipaka ya kisheria.

Amri ya utendaji huenda ikakabiliwa na changamoto za kisheria, kama vile juhudi nyingi za utawala wa Trump kupunguza ukubwa wa serikali ya shirikisho.

Katika hafla ya utiaji saini, Trump alimsifu Linda McMahon, ambaye alimteua kuongoza idara hiyo, na kuelezea matumaini yake kuwa atakuwa waziri wa mwisho wa elimu.

Baada ya Trump kutia saini agizo hilo, Seneta wa chama cha Republican cha Louisiana Bill Cassidy alitangaza mipango ya kuleta sheria inayolenga kuifunga idara hiyo.