
Miaka 30 tangu viongozi wa dunia walipopitisha mpango wa kihistoria wa kufanikisha usawa wa kijinsia, ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa haki za wanawake na wasichana ziko katika hatari kubwa.
Ripoti hiyo, iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na masuala ya Wanawake, UN Women, inabainisha kuwa takribani robo ya serikali duniani zimeripoti kushuhudia kurudi nyuma kwa haki za wanawake mwaka uliopita, huku ubaguzi wa kijinsia ukiendelea kuenea katika jamii na mifumo ya kiuchumi.
Licha ya maendeleo fulani, kama vile upatikanaji wa elimu kwa wasichana na huduma za uzazi wa mpango, bado changamoto ni kubwa. Ripoti inaonyesha kuwa kila baada ya dakika 10, mwanamke au msichana huuawa na mwenza wake au mwanafamilia.
Aidha, matukio ya ukatili wa kingono yanayohusiana na migogoro yameongezeka kwa asilimia 50 tangu mwaka 2022. Zaidi ya hayo, ni nchi 87 pekee ambazo zimewahi kuongozwa na mwanamke, jambo linaloashiria pengo kubwa katika uongozi wa kisiasa.
Soma pia: Lengo la Umoja wa Mataifa la usawa wa kijinsia haliwezi kufikiwa mwaka 2030 kutokana na upendeleo dhidi ya wanawake ulimwenguni
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisisitiza kuwa badala ya kuimarisha usawa wa haki za binadamu, dunia inashuhudia kuenea kwa chuki dhidi ya wanawake. Aliitaka jumuiya ya kimataifa kusimama kidete kuhakikisha haki za wanawake na wasichana zinaheshimiwa kwa wote, kila mahali.
Mwaka 1995, nchi 189 zilihudhuria mkutano wa wanawake wa Beijing na kupitisha azimio la kurasimisha haki za wanawake, likiwataka viongozi kuchukua hatua madhubuti katika maeneo 12, ikiwa ni pamoja na kutokomeza umaskini, kupinga ukatili wa kijinsia, na kuwaweka wanawake katika nafasi za maamuzi. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Umoja wa Mataifa, hati hiyo ilitambua kwamba haki za binadamu zinajumuisha uwezo wa wanawake kuamua kuhusu afya yao ya uzazi na masuala yanayohusiana na maisha yao ya kijinsia bila ubaguzi au shinikizo.