Thursday , 20th Feb , 2025

Oparesheni maalumu ya kuwadhibiti wanyamapori wakali na waharibifu aina ya fisi waliokuwa wanaleta taharuki na madhara Kwa jamii inayoendelea Mkoani Simiyu imeonesha mafanikio makubwa baada ya fisi 16 kuvunwa ikiwa ni hatua muhimu iliyochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili

Oparesheni maalumu ya kuwadhibiti wanyamapori wakali na waharibifu aina ya fisi waliokuwa wanaleta taharuki na madhara Kwa jamii inayoendelea Mkoani Simiyu imeonesha mafanikio makubwa baada ya fisi 16 kuvunwa ikiwa ni hatua muhimu iliyochukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuhakikisha usalama na utulivu Kwa wananchi vinarejea.

Hayo yamesemwa jana Februari 19, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Kenani Kihongosi alipokuwa akiongea na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari.

Mhe. Kihongosi amesema kufuatia changamoto hiyo, Serikali ilichukua jukumu kubwa la kuhakikisha inalinda wananchi wake ikiwemo kuanzisha oparesheni maalumu inayohusisha Jeshi la Uhifadhi Kwa Taasisi za TAWA, TANAPA na TFS Kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wananchi, oparesheni inayotajwa kuanza Januari 25, 2025.

“Tarehe 20, Disemba 2024 baada ya fisi kuvamia wananchi Serikali ilichukua hatua kubwa ya kushirikisha vyombo vyake (TAWA na Jeshi la Polisi) na kuanza Oparesheni, lakini ilipofika tarehe 25, Januari 2025 oparesheni ya mkoa mzima ilifanyika Kwa ukubwa kuhakikisha inakabiliana na fisi wote waliokuwa wanasumbua wananchi” amesema Mhe. Kihongosi

“Na Kwa taarifa njema ni kwamba tangu kuanza Kwa oparesheni hii vyombo vyetu vimeweza kudhibiti na kuua fisi 16 na ndio maana kwasasa mnaweza kuona hali imetulia” ameongeza Mkuu huyo wa mkoa wa Simiyu.

Aidha Mhe. Kihongosi ameendelea kuwatoa hofu wananchi wa mkoa huo akisisitiza kuwa hali ni shwari na kuwataka waendelee na shughuli zao kama kawaida huku akikemea vikali imani za kishirikina kuhusiana na mnyamapori aina ya fisi kwa baadhi ya wakazi wa Simiyu na kuwataka wote wanaofuga wanyamapori pori hao kuacha mara moja kwani ni kosa kisheria kumiliki nyara za Serikali bila Kibali.