
Rais wa Marekani, Donald Trump ameishutumu na kuikosoa Ukraine baada ya rais wake, volodymyr Zelensky kusema kuwa lilikuwa jambo la kushangaza kwamba nchi yake haikualikwa kwenye mazungumzo ya amani huko Saudi Arabia ili kumaliza vita vya Ukraine.
Trump alisema "amekasirishwa" na majibu ya Ukraine na kusema kwamba nchi hiyo"ingeweza kufikia makubaliano"ya kumaliza vita, ambavyo valianza kutokana na uvamizi kamili wa Urusi karibu miaka mitatu iliyopita.
Maoni yake yalifuatia matamko ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, ambaye alisema kwamba nchi yake haitakubali nguvu za kuleta amani kutoka nchi za NATO nchini Ukraine, chini ya makubaliano yoyote ya amani, baada ya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, huko Saudi Arabia.
Urusi na Marekani zilisema kuwa zimekubaliana kutengeneza timu za kuanza mazungumzo ya kumaliza vita.
Akizungumza na waandishi wa habari Trump aliulizwa nini ujumbe wake kwa Ukraine ambao wanaweza kujisikia wamedanganywa. "Nasikia kuwa wamekasirika kwa kutoshiriki, ingawa wamekuwa na nafasi hiyo kwa miaka mitatu na hata kabla ya hapo. "Nadhani nina nguvu za kumaliza vita hivi," alisema Trump.