Saturday , 15th Feb , 2025

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amewahimiza wananchi wa Itilima kujipanga kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CC

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amewahimiza wananchi wa Itilima kujipanga kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025 huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza kama mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Itilima wilayani Itilima mkoani Simiyu Februari 15, 2025, Majaliwa amewataka wanachama wa chama hicho kuendelea kueneza mafanikio yaliyopatikana kupitia Serikali ya CCM ili wagombea wa chama hicho wasipate kazi kubwa katika kampeni.

"Mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu, vyama vyote vitakuja kuomba kura, lakini nyinyi mnajua kuwa CCM inapeleka wagombea wake katika nafasi za Urais, Ubunge na Udiwani. Kwa nafasi ya Urais, mgombea wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kwa Zanzibar ni Dkt. Hussein Mwinyi, huku mgombea mwenza akiwa ni Balozi Dkt. Nchimbi. Watazunguka nchi nzima kuomba ridhaa ya Watanzania," amesema Waziri Mkuu.

Majaliwa amewataka wananchi wa Itilima kuelewa na kushiriki kusambaza taarifa za mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, maji, umeme, kilimo na mifugo, ili kuwawezesha wagombea wa CCM kupita kwa urahisi katika uchaguzi huo.

"Leo mnaelewa kazi iliyofanywa na Serikali yenu na Mbunge wenu. Tunapaswa kuyaeleza haya kwa wengine ili wagombea wetu wasipate kazi ngumu. Wananchi wa Itilima wanapaswa kuwa na uelewa wa hali ya juu kuhusu maendeleo haya," amesema.

Katika sekta ya afya, Majaliwa ameeleza kuwa wilaya hiyo tayari ina zahanati 37, na lengo ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati yake ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

"Tunataka mwananchi apate huduma za afya karibu na makazi yake. Hongera sana Mheshimiwa Njalu Silanga kwa kuhakikisha wilaya hii inapata zahanati nyingi. CCM itaendelea kuhakikisha mbunge wenu anapata ushirikiano wa Serikali ili huduma zote zipatikane hapa Itilima," alisisitiza.

Kuhusu barabara, Waziri Mkuu amekiri kuwa kuna changamoto ya barabara za vumbi, hasa wakati wa msimu wa mvua, lakini akaahidi Serikali kuendelea kuzifanyia maboresho kupitia TARURA.

"Mheshimiwa Mbunge endelea kuwasilisha orodha ya barabara zilizoharibika ili fedha zipatikane na TARURA izitengeneze. Serikali inatambua umuhimu wa barabara katika maendeleo ya wananchi," amesema.

Mkutano huo ulilenga kuwasilisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020/25 jimboni Itilima, huku viongozi na wananchi wakionesha mshikamano mkubwa katika kuunga mkono chama hicho.