Tuesday , 31st Dec , 2024

Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji, Dar es Salaam, kupitia doria zilizofanyika mwezi Disemba, limefanikiwa kuwakamata watu tisa kwa tuhuma za kuvusha abiria kwa njia hatarishi maeneo ya Kivuko cha Ferry jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Kikosi cha wanamaji, ACP Moshi Sokoro akionesha boti zilizokamatwa

Akiongea na EATV, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Wanamaji, Kamishna msaidi wa Jeshi la Polisi, Moshi Sokoro anasema watu hao walikamatwa kwenye doria zilizofanyika Disemba 21 ambapo tuliwakamata watu watano na boto zao pamoja na Disemba  22, tulikamata watu wanne 2024.

“21/12/2024 majira ya saa9:00 alasiri, kikosi cha Polisi wanamaji tulifanya doria maeneo ya kivukoni tukakuta baadhi ya abiria wakisafirishwa kwa njia hatarishi kutoka Ferry Magogoni kwenda Ferry Kigamboni na kufanikiwa kukamata boti tano pamoja na manahodha wake”, ACP Moshi Sokoro, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Wanamaji.

Aidha Kikosi hicho kimefanikiwa kukamata madumu 5655 ya mafuta yakiyokuwa yakisafirishwa kimagendo.
“Tulikamata watuhumiwa wanne ambao walikuwa manahodha wa majahazi manne yaliyokuwa yakisafirisha madumu ya mafuta ya kupikia pasipokuwa na nyaraka muhimu zinazohusu usafirishaji wa mafuta hayo ambalo ni kosa kukwepa ushuru wa forodha”, ACP Moshi Sokoro, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Wanamaji.

Kuhusu wananchi kuvuka maji bila tahadhari baadhi wa wakazi wa Kigamboni wanatoa ushauri kwa wenzao.
“Kama haujui kuogelea hakuna haraka zaidi ya uhai wako, mimi nashauri tusiahatarishe uhai wetu kwa kupanda usafiri usio salama”, Habilal Mwingi, Mkazi wa Kigamboni.

“Ushauri wangu tutumie usafiri ulio rasmi kwa ajili ya usalama wetu kwa sababu, hizi boti ndogo muda wowote zinaweza kupinduka na hazina insurance mwisho wa siku unapoteza maisha",Lilian Valence, Mkazi wa Kigamboni.

“Vile vyombo kwa ajili ya wavuvi sio abiria tuchukue tu tahadhari ya kulinda afya zetu wenyewe ikitokea vile vimebinuka unaweza kupoteza maisha”, Abdallah Mansuri, Mkazi wa Kigamboni.